Chama cha Kiswahili cha laumu wazazi kwa dhana potovu juu ya lugha

By Timothy Mugo

Chama cha Kiswahili kimewalaumu wazazi na baadhi ya waalimu katika ukanda wa ziwa Victoria kwa kudunisha uenezaji wa lugha ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Akizungumza katika hafla ya Kiswahili mjini Migori hapo jana, mwenyekiti na mwanzilishi wa chama cha uchunguzi wa Kiswahili (CHAUKI) Silingi Mulumbi, alisema baadhi ya wazazi katika ukanda wa ziwa Victoria hawazingatii umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa kuwapotosha wanafunzi na wanao kuwa lugha hiyo ni Ngumu jambo ambalo huchangia matokeo duni ya somo la Kiswahili katika mitihani ya kitaifa.

Mwenyekiti huyo alidai kuwa wazazi wengi hawatilii maanani somo la Kiswahili na kufanya wanafunzi na walimu kuwa na dhana na fikira potovu kuhusu Kiswahili.

“Utampata mzazi akimwambia mwanawe kuwa Kiswahili sio ‘mdomo wetu’. Msemo huu huwafanya wanafunzi kukipuuzilia Kiswahili,” Bw. Silingi alidokeza.

Aliwataka wanafunzi na walimu wa somo hilo kuweka bidii ili kutoa dhana hiyo katika jamii zinazoishi ukingoni mwa ziwa Victoria.

Aidha, Mulumbi aliwasuta walimu ambao walitenga siku moja tu ya kuzungumza Kiswahili shuleni pamoja na wale ambao hawakukipa Kiswahili nafasi kuzungunzwa katika baadhi ya shule akisema walilemaza juhudi zilizowekwa za kuimarisha Kiswahili.

Mwenyekiti huyo alisema baadhi ya shule zilipendelea kiingereza saana hata kupelekea wanafunzi ambao walipatikana wakiongea Kiswahili kuadhibiwa vikali.

Mbali na hayo, Mulumbi alisema lugha chipukizi mitaani kamavile ‘sheng’ ilichangia katika kudorora kwa Kiswahili.

“Kunazo pia lugha chipukizi katika mitaa mbalimbali katika ukanda huu ambazo jamii nzima hutumia ambazo zimechangia pakubwa kwa kudunisha Kiswahili,” Mulumbi alisema.

Mulumbi alidai kuwa wanafunzi wengi hukosa nafasi za kupata alama za juu kutokana na kufeli katika Kiswahili na kuchangia katika ukosefu wao wa kufanya taaluma nyingi ambazo pia ni muhimu kama vile waandishi wa habari.

Alisema kuwa eneo la Ziwa Victoria limeshuhudia utata mwingi katika uzungumzi wa lugha hiyo na kufanya walimu na wazazi kuandaa kongamano la Kiswahili miongoni mwa walimu na wanafunzi ili kuweza kupunguza na kutoa dhana hiyo katika akili za wanafunzi wengi.

Mulumbi alidokeza kuwa miongoni mwa wanafunzi wengi katika eneo la Ziwa Victoria wamekuwa wakiwa na matokeo duni kwa kuwa na ukosefu wa maelezo mwafaka kuhusu lugha ya Kiswahili.

Zaidi ya wanafunzi mia tano kutoka shule za msingi za kaunti ya Migori walinufaika na mafunzo kutoka kwa walimu katika kongamano hilo na kupewa vyeti vya kushiriki.

Kongamano hilo liliwaleta pamoja walimu wa shule za msingi, upili na wahadhiri wa vyuo vikuu katika kaunti ya Migori kuweza kutoa dhana potovu katika wanafunzi wengi wa shule za msingi na upili.